Faida za kutumia umemejua majumbani

Picture of Zeph Kivungi

Zeph Kivungi

Director of Learning and Innovation

Faida za kutumia umemejua majumbani

  • Ni pamoja na kuwawezesha watu kujiajiri na kuingiza kipato.
  • Unarahisisha shughuli za mapishi na mwanga nyumbani.

Dar es Salaam.

Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya changamoto kuu zinazoisumbua dunia kwa sasa.

Ili kukabiliana na athari mabadiliko hayo ikiwemo ukame, mafuriko na ongezeko la joto, watalaam wa mazingira wanapendekeza matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia na mwanga.

Nishati hizo ni pamoja na umemejua, umeme wa maji, upepo, tungamotaka, biyogesi ambazo ni rafiki wa mazingira ikilinganishwa na kuni na mkaa ambazo zimekuwa zikidisha tatizo la ukataji wa miti.

Katika makala haya, tunajadili kwa kina nishati ya umemejua na faida zake endapo itatumika majumbani hasa kwa watu waishio vijiji ambako hakuna umeme wa gridi.

Nishati ya jua huundwa kwa paneli zinazokusanya nishati ya mwanga na joto, ambayo huituma kwa mpokeaji anayeibadilisha kuwa nishati ya umeme.

Nishati hii ni chanzo cha nishati mbadala na endelevu, haihitaji aina yoyote ya ubadilishaji wa vifaa kila wakati ili ifanye kazi hivyo gharama za awali za  uwekezaji ni ndogo.

Faida za kutumia umemejua nyumbani

Inasaidia kupata mwanga hasa nyakati za usiku katika maeneo ambayo hayajaunganishwa na gridi ya Taifa na hivyo kuimarisha usalama wa wana kaya ikiwemo kuwaepusha na wadudu wanaoweza kuwadhuru.

Umemejua ni chanzo cha uhakika cha mwanga katika nyumba zetu. Suala la kukatika kwa umeme inaweza kuwa historia ikiwa utaamua kutumia nishati hiyo. Picha | Elico Foundation

“Huku kwetu Serikali bado haijatuletea huduma ya umeme, na siwezi kukaa giza usiku ukiingia nikaona bora nifunge sola ili nipate mwanga na niweze kuchaji simu,” anasema Belina William, mkazi wa Gomvu, Kigamboni, nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Kukosa mwanga wa umeme nyakati za usiku huhatarisha usalama kwa watu kwa kuwa hali hiyo hushawishi wahalifu kufanya kuvamia watu na nyumba, kuiba vitu na kuwadhuru ikiwemo ubakaji.

Umemejua ni fursa

Belina siyo tu anatumia umemejua kupata mwanga, bali anatumia katika shughuli ndogo ndogo za kibiashara ili kujiingizia kipato ikiwemo kutoa huduma ya kuchaji simu ili kuwawezesha watu kuwasiliana.

“Angalau hata kijiji chetu kina maendeleo, biashara ndogo ndogo kama kuchajisha simu zimeanzishwa, wengine wenye mitambo imara zaidi wanaweza hata kupika kwa kutumia umeme huu,” anaeleza Belina huku akihamasisha wananchi wenzake kutumia umemejua.

Pia umemejua hutumika katika shughuli za uzalishaji ikiwemo mashine za kukoboa na kusaga nafaka, vinyozi, mashine za kuchomelea vyuma, kuendesha pump za maji na majokofu ya kugandishia barafu na juisi.

Faida nyingine ya kutumia umemejua ni kuwa baada ya gharama za  awali za ufungaji wa paneli zake, watumiaji wanakua huru kuutumia umeme huo kwa  muda mrefu bila kufanya matengenezo.

Wanaweza kutumia vyombo mbalimbali vya kielektroniki vitumiavyo umeme kama luninga, jikofu, pasi, majiko ya kupikia kwa gharama nafuu sana kulinganisha na ule wa gridi ya Taifa.

Wadau wa nishati jadidifu

Hatua zilizopigwa katika matumizi ya umemejua zimechangiwa kwa kiasi kikubwa na wadau wa nishati jadidifu ambao wamekuwa wakichagiza matumizi ya nishati hiyo kwa kutoa elimu na usaidizi wa kiufundi kwa  Watanzania hasa waishio vijijini.

Shirika lisilo la kiserikali la ELICO Foundation, ambalo linatoa huduma mbalimbali ikiwemo ya mifumo ya umemejua, ni miongoni mwa wadau walio mstari wa mbele kuzifikia kaya ambazo hazijapitiwa na umeme wa gridi ya Taifa.

Hata hivyo, mifumo hii ina gharama zake hivyo si kaya zote zinaweza kuinunua kutokana na changamoto za kiuchumi.

Ili kukabiliana na hali hii shirika limeanzisha mfuko maalum unaoliwezesha kutoa sola hizo kwa mkopo na hivyo kuziwezesha kaya nyingi zaidi kunufaika kwani huruhusiwa kulipia kidogo kidogo.

“Hata hivyo kulingana na ukubwa wa tatizo la upatikanaji wa umeme vijijini, jitihada za wadau wengi zaidi zinahitajika ili kukabiliana na changamoto hii.

“Kama shirika tumefanya kidogo kwa sehemu yetu na tunaamini wadau wengine wanaweza kujifunza kutoka kwetu na kwenda kuwahudumia watu wengi zaidi,” anasema Fredrick Mushi, Mkuu wa Programu na Uendeshaji wa Elico Foundation.

Mikakati ya Serikali

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa nishati inaendelea kuchagiza matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.

Hivi karibuni, Waziri wa nishati January alizunguka katika mikoa 14 na wilaya 38 kutathmini na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kama njia ya kuinua maisha ya Watanzania, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili kuni na mkaa.

Hata hivyo, katika hotuba yake bajeti kwa mwaka 2022/23,  Makamba alisema kwa kushirikiana na wadau, itaandaa na kutekeleza mikakati/mipango mbalimbali ya kuendeleza sekta ya nishati.

Mikakati hiyo ni pamoja na mkakati wa nishati jadidifu, mkakati wa matumizi bora ya nishati na mpango wa utekelezaji na mkakati wa tungamotaka.

Wizara pia itafanya mapitio ya mpango kabambe wa kuendeleza sekta ndogo ya umeme  ili kuhakikisha unaendana na mahitaji ya sasa ya sekta na

“Tutatekeleza mpango kabambe wa nishati vijijini unaohusisha mpango wa usambazaji wa umeme vijijini pamoja na mpango wa nishati safi ya kupikia vijijini,” alisema Makamba katika hotuba hiyo.

Share this on

Other Related