Jinsi taasisi, mashirika yanavyoweza kukwepa mgao wa umeme Tanzania

Picture of Zeph Kivungi

Zeph Kivungi

Director of Learning and Innovation

Betrii za paneli za sola zilizopo nje ya Ofizi ya Elico mtaa wa Makwaiya jijini Dar es Salaam. Picha l Esau Ng’umbi.

Dar es Salaam. ‘Mgao wa umeme’ ni kama wimbo masikioni mwa Watanzania. Si neno jipya tena kwao na mara nyingi litamkwapo basi huambatana na kutopatikana kwa huduma ya nishati ya umeme.

Jiji la Dar es salaam ni miongoni mwa maeneo yanayoathirika zaidi kila tatizo hilo linapoibuka. Jiji hilo siyo tu ni kitovu cha biashara nchini Tanzania na Afrika Mashariki bali viwanda vingi ambavyo utendaji wa shughuli zake hutegemea umeme vipo katika eneo hilo.

Licha ya kuwa kwa sasa hali ya umeme imerejea kama kawaida, Watanzania hawatayasahau machungu ya mgao wa nishati hiyo mwaka 2022 kutokana na kupungua kwa kiwango cha uzalishaji kilichochangiwa na kuchelewa kwa mvua hasa za vuli katika mikoa mbalimbali nchini. 

Wakati athari za mgao wa umeme zikionekana waziwazi kwa kuathiri shughuli zinazohitaji nishati hiyo, je unafahamu kuwa wapo watu ambao hawajaonja adha ya mgao wa umeme, na shughuli zao zinaendelea kama kawaida?

Miongoni mwao ni Shirika la Elico Foundation, taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya upatikanaji wa nishati jadidifu hususan katika maeneo ya vijijini ili kuongeza uzalishaji.

Utathibitisha hilo mara tu utakapowasili katika ofisi zao zilizopo mtaa wa Makwaiya katika Wilaya ya Kinondoni kwa kushuhudia zaidi ya betri 22 za paneli zilizopangwa katika mistari, pembeni tu ya mlango wa kuingia ndani ya ofisi hizo.

Hewa yenye ubaridi wa kubembeleza kutoka kwenye kiyoyozi kilichofungwa ofisini humo ni miongoni mwa starehe niliyokutana nayo baada ya kuingia ndani na hiyo ikanifanya nifungue vifungo vya shati ili kuruhusu mwili wangu kupumzika baada ya kuchomwa na jua kali la Dar es Salaam.

Wakati sauti za majenereta zikisikika katika ofisi zilizo jirani na taasisi hiyo, kuashiria umeme umekatika,  Elico Foundation wao ni kimya tu. Waliamua kuepukana na adha hiyo kwa kutumia umemejua katika ofisi yao. Vifaa vyote vya umeme na kielektroniki katika ofisi hiyo vinatumia umemejua ikiwemo vipozeo, taa, majiko, feni na kompyuta.

Nishati hiyo sio tu imewaepusha na adha ya mgao wa umeme ambayo taasisi nyingine inakumbana nazo bali imewasaidia kuokoa kiasi cha pesa ambacho awali kingetumika kununulia nishati ya umeme wa kukidhi mahitaji ya ofisi yao.

Sisty Basil ni Mkurugenzi Mtendaji wa Elico Foundation ameiambia www.nukta.co.tz kuwa gharama ya kununua umeme ndio iliyowasukuma kufunga mfumo wa umemejua kwani waliamini utasaidia kupunguza makali ya gharama ya umeme.

“Kwa mwezi tulikuwa tunatumia umeme hadi wa Sh600,000 kwa ajili ya kuendesha shughuli zetu za kila siku, tulipopiga hesabu tukabaini tutatumia hela nyingi zaidi kwa siku za usoni tofauti na tukiweka mfumo wa nishati jadidifu ambayo ni umeme jua,” anasema Basil.

Siyo rahisi kukadiria gharama halisi za kufunga mfumo wa umemejua kwani mfumo hufungwa mara baada ya upembuzi yakinifu kufanyika na kubaini matumizi ya taasisi au eneo husika.

“Mfumo wetu ni mkubwa, kwa maeneo ya kijijini unaweza kusukuma hata kaya 120, na sisi tuliupata kutokana na ufadhili kwani gharama yake ni zaidi ya milioni 90, fedha tunazoziokoa kutokana na kupunguza gharama ya umeme zinatumika kwenye shughuli nyingine za ofisi,”  anasema Basil.

Basil anazishauri taasisi mbalimbali kugeukia matumizi ya nishati ya umemejua, jambo ambalo sio tu litapunguza gharama bali litaongeza uhakika wa utoaji huduma zao pamoja na kupunguza uchafuzi wa mazingira 

“Kutumia majenereta kama chanzo cha nishati umeme unapokatika kunaongeza uchafuzi wa mazingira unaochochea mabadiliko ya tabia nchi na athari zake ni kubwa, ” anasema Basil.

Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Tanzania mwaka 2019  lilizindua mfumo wa umemejua uliofungwa katika ofisi zake, maeneo ya Oyster bay, jijini Dar es Salaam, ambao unaozalisha megawati 187 kwa mwaka.

Mtaalamu wa teknolojia wa UNDP Tanzania, Leyla N’Doman anaeleza kuwa wanatumia umemejua kwa asilimia 70 katika ofisi yao na zinazobaki ni umeme wa gridi.

Kampuni ya mafuta ya TotalEnergies nayo ni miongoni mwa taasisi zinazotumia nishati ya umemejua katika kutoa huduma zake kwa baadhi ya vituo vya mafuta ambapo mpaka sasa vituo vyake vinavyotumia nishati hiyo vimefikia 45.

Jiko la umemejua linalotumika kupikia vitu mbalimbali katika ofizi za Elico. Picha | Esau Ng’umbi.

Jinsi unavyofanya kazi

Nishati ya umemejua huzalishwa kupitia paneli ambazo huwa zimewekwa seli za “silicon photovoltaic” (PV) ambazo hufanya kazi ya kugeuza mwanga wa jua kuwa umeme ambao huelekezwa katika inveta ambayo huuchakata na kuufanya kuwa tayari kwa matumizi ya majumbani.

Pamoja na kuwa na vyanzo vingi vya nishati kama umeme jua, upepo,gesi asilia, maji, makaa ya mawe, tungamo taka pamoja na madini ya uraniamu, Serikali ya Tanzania bado imeweka nguvu katika gesi na maji kama vyanzo vya nishati ya umeme.

Nishati inayozalishwa na vyanzo hivyo bado imekuwa haikidhi matumizi kwa nchi nzima hivyo wadau wa nishati wanashauri ni wakati sahihi kwa Serikali kutoa kipaumbele kwa umemejua ambapo kwa mujibu wa Basil kuna uwezekano wa nishati hiyo kuchangia umeme katika gridi ya taifa.

“Kuna kitu kinaitwa net metering, huo ni mfumo ambao utaturuhusu sisi kuuzia Tanesco, sisi hapa mwisho wa juma hatufungui na ikifika saa nne betri zimeshajaa,ni utaratibu ambao umeshaanza kufanyiwa kazi na nina amini utatusaidia kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme,” anasema Basil.

Waziri wa Nishati Januari Makamba alipokuwa akisoma hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2022/23 Bungeni jijini Dodoma aliwaambia wabunge kuwa Serikali imetenga Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kufunga mifumo ya umemejua katika taasisi za umma katika wilaya nane.

“Mradi wa Sustainable Solar Market Packages ni mradi unaoendelea kutekelezwa ambapo unahusisha ufungaji wa mifumo ya kuzalisha umeme jua katika Taasisi za Umma 29 pamoja na kaya katika Wilaya za Biharamulo, Bukombe, Chato, Kasulu, Kibondo, Namtumbo, Tunduru na Sikonge. Kazi zilizopangwa kufanyika ni kufunga mifumo ya umeme jua katika Wilaya zilizosalia za Bukombe na Biharamulo, “ alisema Makamba

Share this on

Other Related