Serikali inatarajiwa kuanza kutekeleza miradi ya umeme wa upepo pamoja na umeme jua katika baadhi ya mikoa Tanzania ikiwemo Shinyanga na Njombe. Picha | Tara energy.
Dar es Salaam. Wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikiendelea kujidhihirisha nchini Tanzania ikiwemo mgao wa umeme unaosababishwa na upungufu wa mvua katika vyanzo vya kuzalisha nishati hiyo, bado nchi ina malengo mlima katika sekta ya nishati.
Miongoni mwa malengo hayo ni kuongeza matumizi ya nishati jadidifu kwa ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa na vyanzo endelevu vya nishati.
Nishati hiyo hutokana na vyanzo vya jua, upepo, maporomoko madogo ya maji, jotoardhi na tungamotaka.
Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akihutubia katika Mkutano wa 27 wa Kimataifa wa Tabianchi (COP27) uliofanyika Sharm el-Sheikh nchini Misri Novemba 2022 alisema pamoja na mambo mengine Tanzania itaongeza matumizi ya nishati jadidifu kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.
“Tutaendelea kuongeza vyanzo vya nishati jadidifu kutoka asilimia 60 mwaka 2015 mpaka asilimia 80 mwaka 2025,” alisema Rais Samia.
Hata hivyo, bado kuna maswali kama kweli inawezekana kwa Tanzania kufikia kiwango hicho ikizingatiwa kuwa imebaki miaka mitatu?
Baadhi ya wadau wa masuala ya nishati walioongea na Nukta (www.nukta.co.tz) wamesema inawezekana kufikiwa kiwango hicho, ikiwa baadhi ya mambo yatafanyika ikiwemo utashi wa kisiasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo kuwa la kiserikali la masuala ya nishati jadidifu la Elico Foundation, Sisty Basil anasema upo uwezekano wa kufikia asilimia hizo kutokana na nguvu kubwa inayotumika na Serikali katika ujenzi wa miradi ya nishati na nishati jadidifu hasa maeneo ya vijijini.
“Kuna miradi mingi inayotekelezwa kama bwawa la Nyerere, mradi wa umemejua Dodoma na Shinyanga na ule wa upepo Makambako naamini itachangia kufikisha asilimia 80 ingawa utekelezaji wake ni wa muda mrefu,” amesema Basil.
Basil anasema wao kama wadau wa nishati wanashirikiana na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati endelevu hususani katika maeneo ya vijijini ili kuongeza upatikanaji wa nishati nchini.
“Tunashirikiana na Wizara ya Nishati ili kubadilisha mitazamo ya watu kuwa hakuna sehemu ambayo nishati ya umeme haiwezi kufika, tunafanya pia tafiti juu ya matumizi ya nishati ya umeme kupikia pamoja na gesi ya Ethanol, hii ni sehemu ya mchango wetu, ” anasema Basil.
Sera ya Nishati ya mwaka 2015 imesisitiza kuweka juhudi katika kuendeleza sekta ya nishati jadidifu mpaka kufikia asilimia 50 mwaka 2025 ili kuchochea upatikanaji wa nishati ya uzalishaji nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea) Mhandisi Prosper Magali anasema kuwa kutokuwepo kwa sera ya nishati jadidifu ni miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma mchango wa sekta hiyo katika upatikanaji wa nishati.
“Kwa sasa tunaendelea na uandaaji wa mpango mkakati wa nishati jadidifu lakini tumeishauri Serikali kuwa mkakati unatakiwa utoke kwenye sera ya nishati jadidifu ambayo ingeainisha miongozo ya kuikamilisha, “ anasema Magali.
Mhandisi Magali anaamini kuwa ili kukamilisha hilo ni muhimu Serikali ikatanua wigo na kushirikiana na sekta binafsi ambayo itaongeza nguvu kwa kuwekeza katika sekta ndogo ya nishati jadidifu.
“Kuna mipango inayoendelea ya kuvutia sekta binafsi kuwekeza kwenye nishati jadidifu, inaweza kuchangia kufikia huko, kuna miradi ya umemejua pamoja na upepo ambayo inatarajiwa kutekelezwa,” anasema Magali.
Magali amekiri kuwa kauli ya Rais ni kiashirio kwamba sasa Serikali imelitupia jicho nishati jadidifu ambapo amesisitiza kauli hizo zijikite katika vitendo ili kuboresha sekta hiyo ambayo itachangia upatikanaji wa nishati.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo yana vyanzo vingi vya nishati jadidifu lakini bado havijapewa kipaumbele kutokana na gharama kubwa za uzalishaji.
Waziri wa Nishati Januari Makamba alipokuwa akisoma mipango ya utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2022/23 mapema mwaka jana aliwaambia wabunge kuwa miongoni mwa vipaumbele vya bajeti hiyo ni utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu
“Kutekeleza miradi ya nishati jadidifu ikiwemo jotoardhi, tungamotaka, upepo na jua pamoja na matumizi bora ya Nishati (Energy Efficiency and Conservation),” inasomeka sehemu ya hotuba hiyo.